UKOMBOZI WA FIKRA
Mara baada ya kupata Uhuru wa Bendera, Mwl. Julius Nyerere alielekeza nguvu katika Uhuru wa Fikra maana aliamini bila Ukombozi wa Fikra, watanzania wataendelea kuishi utumwani. Kwahiyo akapeleka vijana wengi karibu kila kona ya dunia kuutafuta Ukombozi wa Fikra kupitia elimu. Lakini kwa bahati mbaya wengi wakaenda kupambana na mitihani badala ya ujinga. Wakarudi na fikra hatarishi kwa rasilimali za nchi. Mpaka mwalimu anaondoka duniani watanzania bado tunamwayamwaya katika Uhuru wa Bendera. Mwalimu katuachia uhuru ambao mwenye nacho ndio binadamu na asiyenacho ni takataka. Uhuru wa wachache kuishi kama malaika na wengi kuishi kama mashetani. Uhuru unaowagawa watu kwa kipato na elimu. Uhuru wa bendera ni sawa na kuvaa suruali isiyo na zipu harusini. Uhuru wa bendera umetujengea nidhamu ya woga kwa manufaa ya wachache kutunyonya kutokana na uoga wetu. Tunahitaji uhuru kamili. Ule uhuru unaoanzia kichwani, yaani uhuru wa fikra. Uhuru utakaotusaidia kuyaona mambo katika uhalisia wake. Kichwani pakiwa vizuri hatutapoteza muda kukimbizana na samaki bwawani kama tunataka kuwakamata. Badala yake ni kuwakaushia maji yote tu. Kumbuka “Fikra zinazoongoza akili yako ni muhimu zaidi ya kiasi cha akili ulizo nazo,” alisema David J. Schwartz kupitia kitabu chake cha, “The Magic of Thinking Big.” Fikra sahihi zinahitaji utulivu wa akili. Kuwa na muda wa kufikiri ndilo chimbuko la maendeleo yote duniani. Tunahitaji kuwa na karakana za kufikiri akilini. Badala ya kufikiri umaskini tulionao ni mapenzi ya Mungu, tufikiri umaskini kama matokeo ya kutofikiri vizuri. Mungu ametupa rasilimali nyingi ambazo kama zingelitumika kwa faida yetu, zingeliweza kutuinua tukawa matajiri. Tufikiri kwanza ndipo tutende. Kwame Nkrumah alisema, “Matendo pasipo mawazo ni upofu, mawazo pasipo vitendo ni utupu.” Kumbe saa ya ukombozi wa fikra ni sasa. Tusitegemee kama kuna mtu atakuja kutukomboa isipokuwa ni sisi wenyewe aliimba Bob Marley katika kibao cha, “Redemption.” Bila fikra huru tutaendelea kushuhudia watawala wakishindana katika matanuzi. Akinunua BMW, mwenzake ananunua Benz. Hii ndio itikadi ya Bongo. Kumbuka, “Leo upo pale ambapo mawazo yako yamekuleta, kesho utakuwa pale ambapo mawazo yako yatakupeleka. Mtu anavyofikiria katika akili yake anakuwa hivyo, na anavyochagua anakuwa hivyo.” Kumbe tuna kila sababu ya kuchagua kufikiri vizuri ili kuwa na taifa lenye maendeleo. Hivyo basi jiongezee maarifa kwa kusoma kitabu hiki na hakika utakombolewa kifikra. Mfalme Sulemani alisema, “Akili ya mtu mwelevu hutafuta maarifa na sikio la mtu mwenye busara hutafuta kusikia maarifa.”
Denis Mpagaze ni mwandishi mashuhuri wa makala za viongozi na msuala ya kijamii kama vile ndoa, elimu, maisha, biashara, mapenzi, tamaduni, imani na dini. Makala nyingi za Mpagaze husimuliwa na Ananias Edgar kupitia mitandao ya kijamii na redio mbalimbali. Kabla ya kujikita katika uandishi, Mpagaze alikuwa mwalimu wa chuo kikuu cha Mt. Agostino cha Tanzania yaani SAUT kwa zaidi ya miaka 12 lakini aliamua kuachana na ajira na kufanya shughuli za kuitumikia jamii ya kiafrika. Andika DENIS MPAGAZE katika Youtube na utaona kazi zake nyingi!
Sold by: Lackson Tungaraza
Sold by: Lackson Tungaraza
Sold by: Lackson Tungaraza
Sold by: Lackson Tungaraza