UCHUMI NA KANISA LA LEO
Inapohusu suala la mafanikio, kila mtu anatamani kuwa nayo na kila uchao watu wanapishana huku na kule wakitafuta fursa za kufanikiwa kiuchumi. Lakini ukweli ni kwamba si jambo rahisi kuyafikia mafanikio na uhuru wa kiuchumi bila kumshirikisha Mungu ambaye ndio mwasisi wa uchumi ,Mungu akasema, Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi "Mwanzo 1:26.Hatuwezi kufanikiwa kiuchumi bila kuweka mikakati mizuri na malengo thabiti, juhudi na maarifa. Mafanikio ya kiuchumi yana kanuni na taratibu zake na njia zake.
Kitabu hiki cha UCHUMI NA KANISA LA LEO kimeandaliwa maalumu kwa ajili ya kumsaidia mwamini kupata misingi itakayomwezesha kukua kiuchumi kwa kupitia kujua utimilifu wa ahadi za Mungu kwa mwanadamu juu ya uchumi kupitia kuteswa kwake kristo " kwa kupigwa kwake sisi tumepona". Kwa sababu ya ustawi kiroho na kimwili, kuna umuhimu mkubwa sana kwa mwamini kujifunza suala la uchumi. Mwanadamu ana mahitaji ambayo hayaishi na huwa yanakawaida ya kujirudia mara kwa mara kwa mfano mahitaji ya chakula, mavazi, mawasiliano, usafiri, matibabu na huduma za kila siku kama umeme, maji na kulipia gharama za elimu kwa watoto. Kanisa linahitaji fedha kwa ajili ya kuendeleza kazi ya kuujenga ufalme wa Mungu. Waumini wa kanisa wanahitaji uchumi ili waweze kuhusika katika ujenzi wa kanisa na kuchangia huduma mbalimbali ndani ya kanisa. Waumini wana mahitaji ya kila siku, mahitaji yanayowafanya wakati mwingine licha ya kuwa na moyo mzuri, wanashindwa kushirika shughuli mbalimbali zinazogusa eneo la uchumi Kama vile sadaka, fungu la kumi, michango ya ujenzi na maendeleo, kuwatunza watumishi wao, kama wachungaji na walimu wao pamoja na kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii. Dhima kuu katika kitabu hiki ni kuleta mabadiliko chanya kwa kanisa la leo na kumsaidia mkristo kujua misingi ya uchumi na ahadi za mungu kupitia biblia takatifu. Aidha kukuza ari ya kujitambua, kujithamini, kujiamini, kuthubutu na kuamua kuanza kuchukua juhudi za makusudi kufikia uchumi mkubwa.