TAFADHALI USIFE - SEHEMU YA 01
Hadithi ya kusisimua yenye visa bunifu vya kukuburudisha,kukuelimisha na kukutahadharisha! Soma ushangazwe.
Ghafla ujumbe wa simu uliingia katika simu ya Pauline, ulikuwa ni ujumbe uleule wenye maneno yaleyale uliokuwa ukimtesa siku zote. Palepale hali ikaanza kubadilika,joto lilipanda na jasho likaanza kumtiririka kama maji ya msimu. Taratibu akaanza kulegea huku damu nyingi zikianza kumvuja katika sehemu zake za siri.
Japokuwa alikuwa ameshajiandaa kukabiliana na hali ile kwa kujua kuwa hali ile ingemtokea wakati wowote ule, lakini hakupenda kabisa hali ile kumtokea akiwa safarini. Kuna wakati alimlaumu Mungu kwa kutomsaidia kuondokana na hali ile.Bila kutoa sauti alilia kwa uchungu mkubwa mno!
Abiria aliyekuwa pembeni yake alihisi kuna tatizo linalomkabili abiria mwenzie. Akajaribu kumuita Pauline lakini hakuitika na wala hakujua kama kuna mtu alikuwa anamuita.
Abiria yule mwanamama wa makamo alihisi kuna jambo baya linalomtesa binti yule. Alimuangalia kwa huruma nyingi. Alipoendelea kumuangalia kwa makini kumbukumbu fulani zilipita kichwani mwake. Ingawa Pauline alikuwa amejitanda ushungi mweusi akiwa katika hali ya kutojitambua, bado mama yule aliendelea kuvuta kumbukumbu zake kupitia sehemu ndogo ya uso wa Pauline iliyoachwa wazi na ushungi ule......Aaaaaah, mama yule alipiga ukelele kwa nguvu. Kuna jambo kubwa alilitambua.....................