Tabasamu La Huba
Riwaya inayohusu: Mapenzi ya dhati na kujitoa mhanga.
Tabasamu la Huba ni hadithi ya kusisimua, inayomuelezea mwanadada Rasab, anayekutana na kijana Rifad. Lakini kuna siri kubwa aliyonayo Rasab kuhusu maisha yake....
****************
Nilitazama albamu kuanzia mwanzo hadi mwisho, na nilirudia tena na tena bila kuchoka. Hadi macho yangu yalivyoanza kuona kiza kwa ajili ya machozi yaliyokuwa yakinitiririka mfululizo. moyo ulinienda mbio na jasho jembamba lilikuwa likinitoka. Sikuweza kuendelea tena ndipo nilipofunga albamu langu na kujilaza katika sofa kubwa nililokuwa nimekaa. Nilijipumzisha dakika kama thalathini, nilifumba macho sikuweza kuona mazingira ya kawaida, lakini akili yangu ilienda mbali na kufikiri mambo yote yaliyopita miaka kumi.
Nilimuomba Mungu anisaidie nisahau yote a nikubali niliyokuwa nayo kwa sasa. kwani sikuwa na njia ya kukubali ukweli ulivyo, subira ilihitajika mno na kama mnavyojua subira ni ngumu. Moyo wangu ulikuwa unawaka kwa huzuni nilizokuwa nazo. Sikujua nini cha kufanya ili niondokane na huzuni hizo zilizouchana kabisa moyo wangu. Na kuungika kwake kulitaka nipate faraja, mapenzi ya dhati, huruma na nipate mtu atakayenijali na kunithamini jinsi nilivyo.
Siku hiyo ilikuwa ni siku ya kutimiza miaka ishirini ya ndoa ya dada yangu na mume wake. kwa hiyo nilikuwa nimealikwa katika sherehe yao hiyo. Dada yangu Suad alikuwa ndiye ndugu yangu wa pekee. Kwani tulikuwa tumezaliwa wawili tu, mimi nikiwa ni mdogo wake kwa miaka kumi. Mama alichelewa sana kuchukua ujauzito wangu, mwisho alifikiri hatopata mtoto mwengine zaidi ya dada yangu. Lakini kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu nilikuja mimi duniani.