SAFARI YA KUZAMIA AFRIKA YA KUSINI KWA NJIA ZA PANYA
Kwa muda mrefu vijana kutoka katika maeneo mbalimbali ya bara la Afrika wamekuwa na ndoto ya kufika katika nchi ya Afrika ya kusini ili kuweza kujaribu bahati zao za maisha. Nchi hiyo ambayo inapatikana katika eneo la kusini mwa bara la Afrika imekuwa ni kivutio na kitovu cha wahamiaji wengi kutoka katika mataifa yote ya bara la Afrika na mabara mengine. Ni nchi ambayo ina mambo mengi yenye historia kubwa ambayo haiwezi kusahaurika kwa vizazi vya sasa na vijavyo. Kutokana na historia ya kuvutia, siasa na uchumi imara wa nchi hiyo vijana wengi kutoka katika maeneo mbalimbali ya bara zima la Afrika wanataka kutimiza ndoto zao za kuhakikisha wanafika katika nchi hiyo ili waweze kupata ajira na kuishi maisha mazuri. Kumekuwa na msukumo mkubwa wa vijana kutaka kuzamia katika nchi hiyo bila ya kufuata taratibu zinazokubarika na zilizowekwa kwa mjibu wa sheria. Ni msukumo huo ambao unafanya kijana wa Kitanzania kuianza safari yake ya kuelekea Afrika ya kusini kwa njia za panya zinazoambata na hatari nyingi ambazo zinakaribia kabisa kuitoa roho yake. Anapata misukusuko mingi ambayo inampelekea kuwa mharifu wa kimataifa ambae anatafutwa na mataifa matano ya Tanzania, Zambia, Malawi, Zimbabwe na Afrika ya kusini kwa makosa mabalimbali ambayo kama atakamatwa hawezi kuikwepa jera. Pia katika harakati hizo anajikuta katika magenge ya wauza madawa ya kulevya na waasi wanaopigana dhidi ya serikali ya jamhuri ya kidemokrasia ya kongo, makundi haya yameapa yakimpata yatahakikisha yanamuangamiza. Fuatilia jinsi kijana huyo wa Kitanzania alivyo pambana kuvikwepa vikwazo vyote na hatimae kujikuta yupo katika moja ya nchi Tajiri duniani huku akiwa anayafurahia maisha yake.
Mimi ni mtanzania mzaliwa wa Mbeya. Kwa sasa umri wangu ni wa kutosha kidogo kwa sababu nipo duniani tangu miaka ya 1980. Wakati nasoma shule ya msingi kwenye miaka ya 1990 hivi tulikuwa tunaimba nyimbo maarufu wakati huo za kupinga ubaguzi wa rangi uliokuwa unafanywa na serikali ya makabulu kule Afrika ya kusini. Tuliimba nyimbo hizo kwenye Mchakamchaka, mistarini (Assemble) na kwa kutumia kwaya ya shule. Kwa kweli zile siku za madarasa ya mwanzo ya darasa la kwanza hadi la tatu sikuwa naelewa sababu za kuimba nyimbo zile ni nini na hata Afrika ya kusini yenyewe ni kitu gani.
Nilipofika Darasa la nne nilikutana na rafiki yangu wa muda mrefu aliyeitwa Gilbert Simya na ambae kwa wakati ule alikuwa darasa la saba na alikuwa ndio mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa zaidi kitaaluma katika darasa lao.
Kwa kuwa nilikuwa namuamini sana kwa ujuvi wa mambo mbalimbali, niliamua kumuuliza ni kwanini tunaimba zile nyimbo za kupinga ubaguzi, uliokuwa unaendelea nchini Afrika ya kusini na je Afrika kusini ni nchi gani? Ndugu Simya alinieleza sababu ya sisi kuimba zile nyimbo kwa kina sana na zaidi aliweza kunieleza kwa kina kwamba Afrika kusini ni nchi inayopatika eneo la kusini mwa bara la Afrika.
Ili kunielewesha zaidi na vizuri alinionesha ramani ya Afrika kwenye eneo linaloonesha nchi ya Afrika ya kusini na kwa hakika nilimuelewa sana bwana Simya. Jambo ambalo nalikumbuka sana katika yale mazungumzo yetu ni kwamba baada ya yale mazungumzo yetu nilianza kuipenda sana nchi ya Afrika kusini.
Niliendelea kufuatilia habari za Afrika ya kusini kutoka kwa walimu na Redio ya Sauti ya Ujerumani (DW) na vyombo vya habari vya hapa nchini tangu wakati ule na hata baada ya uhuru wao mwaka 1994.
Nilipomaliza darasa la Saba tayari nilikuwa nimeshakata shauri kwamba lazima nitatafuta fedha ili niende Afrika ya kusini. Nilijiapiza kwamba siku nitakapo bahatika kwenda Afrika kusini nitakwenda kufanya kazi kabisa na ikiwezekana nitakaa moja kwa moja bila kurejea tena Tanzania. Hivyo, nikaanza kujiandaa kutimiza hiyo ndoto yangu ya Muda mrefu.
Katika kipindi chote ambacho nilikuwa nasoma sekondari, yaani miaka minne ya o-level, nilikuwa najiandaa kwa safari yangu kiujuvi, kirasilimali na kisaikolojia. Baada tu ya kumaliza kidato cha nne, mwaka 2003, kabla hata matokeo hayajatoka, niliamua kuanza safari yangu ya kwenda Afrika ya kusini na malengo yangu yalikuwa ni kufika katika jiji la Johannesburg.
Story hii inaeleza visa na mikasa ya safari za watu wanaojaribu kwenda Afrika ya kusini bila ya kufuata utaratibu, kwa kiasi kikubwa nimejivika uhusika mimi mwenyewe ili kunogesha stori hii.
Kwa hiyo, utaweza kusoma safari zangu zote mbili ambazo inaonekana nilizifanya kati ya mwaka 2004- 2006.
Naamini wasomaji wa stori hizi hasa watu ambao bado wana ndoto za kuzamia Afrika ya kusini watakuwa na jambo la kujifunza katika safari zao.