Your Basket

Checkout | Shopping Cart
Nimekusamehe Ila Sitakusahau - GetValue
Biashara & Ujasilimia Mali

NIMEKUSAMEHE ILA SITAKUSAHAU

0
0
  • 5
  • 4
  • 3
  • 2
  • 1
Price:
3,000 Tsh.
Vendor:
Added To Cart:
0
Added to shop:
Aug 11, 2023
Product Views:
1,300
In category:
Sample

Simulizi ya Kusisimua

*NIMEKUSAMEHE ILA SITASAHAU* *SEHEMU YA 01---05*

"uuuwiiiii Diana mambo gani hayo ya kumwagiana maji mdogo wangu??!" nililalamika lakini siyo kwa kumaanisha au kwa kutokupenda ila ni kwa sababu maji yalikuwa ya baridi aliyokuwa ananimwagia mdogo wangu Diana

"hakuna cha mambo gani wala mambo gani hapa unaoga maji tu Happy birthday to you my sister!!" Diana aliniambia huku akinimwagia maji kwa mpira alioninyang'anya wakati nikiwa namwagilia bustani asubuhi, mimi mwenyewe sikukumbuka kama ni siku yangu ya kuzaliwa, niliamka tu na kuanza shughuli zangu za kila siku,

Diana mdogo wangu aliyekuwa amejiandaa kwenda chuoni ndiye aliyenikumbusha kama kuna sikukuu yangu ya kuzaliwa leo

"kumbe ni my birthday leo uuwiii jamani nimesahau kabisa mdogo wangu asante!" nilimwambia nikitaka kumkumbatia

"we we we dada ishia hapo hapo unamkumbatia nani?" alininyooshea kidole
"jamani kwani dhambi kukukumbatia?" "na ulivyolowa hivyo naenda chuoni mwenzako nimeshajiandaa utanilowesha bure!"

"hahaha si nimesahau na ningekulowesha kweli usistaduu wote ukuishage"

"thubutuu!!" nakuvuta nywele "huweze wapi"
"haya dada mimi naenda ila baadae nakuletea kitu kizuri nikirudi chuoni" "kitu gani jamani?"

"supriseee we subiri tu utaona" "jamani nidokeze hata kidogo yaani hapa unanipa kimuhemuhe"
"wait and see my dear sister (subiri uone dada yangu mpendwa)" aliniambia akinibusu shavuni na kuondoka mbiombio akiita bodaboda na kuondoka akiniacha natabasamu tu peke yangu nikiwa nimelowana chapachapa asubuhi asubuhi na ndipo niliposikia hatua za viatu nyuma yangu nilipotazama nikamuona mume wangu George akiwa ametoka amejiandaa

anaelekea kazini nikamfuata kimahaba na kumshika begani

"taratibu utanichafua" alinizuia nisimshike begani
"ni maji tu mume wangu mpenzi ndo umeshajiandaa hivyo, mbona umebadilisha shati nililokuvalisha na tai yake umevaa shati jingine?"

"nimeamua tu tutaonana baadae!" alinijibu na kulifuata gari
"mume wangu" nilimfuata
"nawahi kazini Rebecca tutazungumza nikirudi"

"leo ni siku gani unakumbuka?"
"ni ijumaa leo"
"kuna tukio gani?"
"Rebecca baadae unanichelewesha"

"ni birthday yangu jamani mume wangu"
"happy birthday to you" aliniambia huku akifungua mlango wa gari
"ndo ya juu juu hivyo jamani?" "nikirudi Rebecca" alinijibu akawasha gari nami sikuwa na cha kufanya nilimuaga tu kwa kumpungia mkono wakati akiondoka na gari akionekana anawaza mbali mimi kama namsumbua tu lakini nilijua ni uchovu tu wa jana maana alichelewa kurudi alirudi saa tano usiku akiniambia kulikuwa na kikao cha dharura ofisini kwao

"mama"
"mumy!" watoto wangu waliokuwa wameshaandaliwa na dada wa kazi waliniita wakiwa tayari kwenda shule na sare zao na mabegi yao mgongoni

"naam wanangu wazuri!"
"happy birthday to you happy birthday to you happy birthday dear mamy happy birthday to youuu!" waliniimbia na kunikumbatia na dada wa kazi aitwae Aisha karibia waniangushe chini

"asanteni sana wanangu wazuri"

"haya bye mamaa!"
"mniletee zawadi"
"haya mama" walinijibu wakienda barabarani kusubiri gari lao la shule (school bus) nilikuwa na watoto watatu, wa kwanza Theresia akiwa darasa la saba, Robert darasa la nne na binti yangu mdogo Leticia akiwa chekechea

Waliondoka na dada wa kazi wote wakisoma shule moja, nami nikaendelea kumwagilia bustani nje ya nyumba yangu

"hodi hodi humu ndani"
"karibu sana" nilimwitikia mgeni huyo ambae alipishana na watoto wangu getini hakuwa mwingine ila ni mwanamama Magritha, rafiki yangu wa karibu ninayesali nae kanisani na tukiwa wote kwenye Saccoss moja ya wanawake

"naona vijana wanaenda shule"
"eeh karibu sana namimi namwagilia bustani hapa"
"Rebecca unachekesha kweli yaani badala ungepanda mboga mboga ule

wewe unamwagilia bustani ya maua uwafaidishe nyuki mimi siwezi kazi kama hiyo"
"nyumba inapendeza bibi wee karibu kiti barazani"

"hapa pananitosha siwezi kuingia ndani huko asubuhi yote hii sitaki chai za watu ndokwanza saa kumi na mbili" aliniambia akikaa kwenye mawe ya bustanini

"enhee za asubuhi"
"njema Rebecca za kwako na familia?" "safi kabisa nipe habari naona asubuhi asubuhi"
"nimekuja uniazime elfu hamsini tu shoga yangu wala nisizunguke zunguke nipo vibaya mwanangu anadaiwa shuleni ameshindwa kwenda leo yaani"

"mh Magreth sina hata akiba humo ndani"
"jikung'ute tu shoga yangu naaibika mwenzio, nitakurudishia jumapili kanisani kuna hela yangu kwenye Vicoba tunavunja jumapili"

"sawa ngoja nikakuchukulie hela fulani ina kazi nyingine ila kazi yake ni ya wiki ijayo"
"nashukuru sana"

"usijali tumetoka mbali sana" nilimjibu nikiinuka kutaka kwenda ndani

"Rebecca!" aliniita
"abee" nikageuka
"mumeo yupo?"
"ameenda kazini"
"mmh jana alirudi saa ngapi?" "kwanini unauliza?"

"nauliza tu kuna ubaya?"
"alirudi saa tano hivi na nusu karibia saa sita usiku"
"ohoo na mdogo wako yule Diana alirudi saa ngapi?"

"mbona maswali jamani Magreth rafiki yangu?"
"swali la mwisho tu hili"
"alirudi kama saa tano hivi na yeye walipishana kidogo tu na shemeji yake ila Diana alitangulia kama robo saa hivi kabla ya shemeji yake"

"vipi hujahisi kitu chochote kutokana na maswali yangu na hiyo mida niliyokuuliza?" Magreth aliniuliza nikabaki njiapanda nikishindwa kumuelewa anamaanisha nini kuniuliza maswali hayo

"hapana nifafanulie"
"jana nimewaona mumeo na mdogo wako pamoja kwenye mazingira nisiyoyaelewa elewa!!"

"unasema???!!".... *SEHEMU YA 02*

"unasemaje sijakuelewa?" nilimwuliza Magreth
"nimesema hivi mbona jana nimemkuta mdogo wako na shemeji yake kwenye mazingira yasiyoeleweka"

"mdogo wangu gani?"

"kwani una wadogo wangapi hapa mjini Rebecca unaoishi nao?"
"nina mdogo wangu mmoja tu, Diana"

"basi huyo huyo"
"mazingira yasiyoeleweka kama yapi?" "eeh wewe chunguza tu mwenyewe sitaki kufungwa mie bure" "hujaachaga tu uchonganishi Margrth rafiki yangu unakumbuka ulitaka kusababisha ndoa ya mzee wa kanisa yule mama kuvunjika kanisani?"

"lakini si lilikuwa la kweli lile jambo nililoongea Rebecca au nilikosea jamani kuufichua ukweli?"

"umewafananisha tu mdogo wangu Diana alikuwa chuoni kwenye sherehe na rafiki zake na shemeji yake alikuwa

kwenye kikao cha dharura ofisini kama wangekuwa wote basi wangerudi pamoja hata wangesingizia tu kuwa wamekutana njiani sipendi maneno maneno mimi sikuhizi Magreth"

"mh haya nileteage mie hiyo hela niende zangu, mdomo koma!" Magreth aliongea nikatikisa kichwa kumsikitikia kwa tabia yake ya umbea mpaka sikuhizi nimepunguza uswahiba nae tofauti na zamani nilipokuwa swahiba wake mkubwa, yote kutokana na mdomo wake huo uliokuwa kama cherehani, halimpiti jambo kashalijua na kulisambaza hasa kwangu, sasa isije ikawa na yangu anayasambaza kwa wengine hivyo nikawa simwambii kila kitu kuhusu maisha yangu

Niliingia ndani na kuchukua kiasi cha pesa elfu thelathini nilichokuwa nacho, nikatoka na kumpatia, akanishukuru na wala sikutaka anilipe kwa sababu tulisaidiana sana hasa kipindi kile nilipokuwa sina kitu nilipoolewa na kuhamia kanisani kwao ambapo alikuwa anasali mume wangu kabla hajanioa

"leo nimezaliwa mwenzio" .
"waaoh dah happy birthday to you shoga yangu ila siku imenikalia vibaya sina hata zawadi jamani?"

"usijali we njoo tu baadae jioni zawadi ya pekee ninayoitaka kutoka kwako ni kukuona baadae jioni nitaandaa chakula kizuri sana"

"vipi kitimoto itakuwepo?" alininong'oneza sikioni akiwa ni mpenzi sana wa kitoweo hicho

"sikupanga lakini kwa sababu nina uhakika upo nitatengeneza special for you yaani"

"uuuwiii lazima nije kuchambua mchele kabisa utanipigia basi ngoja niende nikalipe lipe najua sitakosa elfu ishirini"

"haya kwaheri" nilimuaga huku nikibaki natabasamu nikafunga bomba la maji na kurudi ndani kuendelea na mipango mingine ya usafi nikisaidiana na dada wa kazi Aisha

Siku ilienda hivyo nikiwa nimeshinda nyumbani tu sijaenda kwenye biashara yangu ya saluni kwa sababu ya mambo kadhaa ambayo hayajakaa sawa na siku chache zilizopita niliumwa umwa, mdogo wangu Diana alirudi kutoka chuoni tukasalimiana na moja kwa moja akaingia mpaka chumbani kwake, nikiishi nae na kumsomesha mimi mwenyewe tangu sekondari, kidato cha tano na sita mpaka sasa yupo chuoni mwaka wa mwisho

Nilipita chumbani kwake na kumsikia akiongea na simu maana nilitaka kumuita nimuagize

"mh kaninunulia bonge la simu yaani ngachoka, nilidhani itakuwa zawadi ya kitoto sijui ya vi infinix sijui nini shoga

siyo infinix wala tekno wala samsung yaani simu ya hatari wanayotumia mastaa mbona chuoni nitavimba" nilimsikia nikavutiwa na maongezi yake kama dada mtu nikataka umbea kidogo nikafungua mlango na kumkuta amekaa kitandani kwake haraka akakata simu aliyokuwa anaongea na rafiki yake huyo

"yaani Diana hata kunionyesha mimi dada yako hayo mambo mazuri unaanza kwa marafiki jamani, shemeji yangu nini?" nilimchungulia mlangoni sikuingia kabisa

"utaiona dada yangu wewe tena"

"mbona hunionyeshi hata kwa picha shemeji yangu nimjue umelete hata nyumbani siku moja tule nae chakula

maana anajitahidi kaka wa watu kila siku nakuona na magauni ya bei mbaya na maviatu, utulie Diana usiruke ruke kijana wa watu utamuua kwa presha"

"hahaha dada bwana kwani unaniona mimi mcharuko au??" alicheka na kijikaratasi kimoja kikapeperuka kutokana na upepo wa feni aliyoiwasha kikanifikia mguuni nikakiokota na kukisoma, ilikuwa ni risiti, ilionyesha bei ya simu na aina ya simu, vyote vikanishtua nikamtazama Diana ambae alipogundua nimeshika karatasi yake akaja na kuninyang'anya

"Diana simu ya milioni mbili??"
"dada kawaida tu unaionaje si Iphone macho matatu hii tena kuna toleo

mpaka la ngapi sijui huko" alinionyesha boksi la simu hiyo

"hela unapata wapi?"
"si mchumba wangu nawewe?"
"sasa si ungemwomba akufungulie biashara"
"atanifungulia tu hili trela"
"mh haya, hayanihusu chakula kipo jikoni"
"nimeshiba dada nataka nilale tu" "sawa" nilimjibu na kuufunga mlango wake na ndipo nilipokutana na mume wangu Dawson nae alikuwa ndo anaingia, nikampokea begi na kulipeleka chumbani nikalitua na kutaka kumfungua vifungo vya shati

"acha tu nitavua mwenyewe" aliniambia

"pole na kazi mume wangu"
"asante" alinijibu akavua suruali yake wakati anataka kuitundika kwenye henga kijikaratasi kikaanguka akiwa hajakiona mimi nikainama na kukitazama kilikuwa ni cha maelekezo ya jinsi ya kutumia simu lakini simu yenyewe niliyoina kwenye kikaratasi hicho ni kama ile mpya niliyoiona kwa mdogo wangu Diana sambamba na eyerphones zilizoandikwa jina la simu lilelile kama ya Diana....

*SEHEMU YA 03*

"kinini hiko unachokitazama" alinifuata na kuninyang'anya haraka haraka mkononi mpaka nikaingiwa na wasiwasi

"mme wangu umenunua simu kwani?" "wewe unataka ujue ili iweje, sijanunua"
"mh sasa hizi earphones na maelekezo ni ya nini?"

"sasa mbona una haraka Rebecca si usubiri au umesahau leo ni siku gani jamani?"

"halafu sipendi unavyoniita Rebecca mimi ni nani wako kwani?"
"aah nisamehe mke wangu kipenzi wakati mwingine nalimisi jina lako halisi nililolizoea wakati ule kama sijakuoa mmwaaah" alinijibu na kunibusu shavuni nikatabasamu

"utakula, nikutengenezee nini?" "nimeshiba, nitasubiri cha jioni tu mke wangu" alinijibu na muda huohuo

tukasikia sebuleni wanaimba wimbo wa happy birthday to you happy birthday to you kana kwamba kuna watu wengi ikabidi nitoke kuja kutazama ni wageni gani hao nikamkuta rafiki yangu Margreth amekuja na wanawake wengine kutoka kwenye Saccoss yetu wameniletea keki nzuri wameiweka mezani na watoto wangu watatu, Theresia, Robert na mdogo wao wa mwisho, Leticia wakiwa wamesharudishwa na gari wakiwa na sare zao za shule

"waaaoh jamaniii!" nilijiziba mdomo baada ya kufanyiwa suprise hiyo na mume wangu nae akatoka, walikuwa wamekuja na makreti ya soda na vitafunwa (bites) na majirani zangu kadhaa nao niliwaona lakini mdogo

wangu Diana alikuwa chumbani kwake hakutoka, mume wangu aliwasalimia na kurejea chumbani maana simu yake iliita akaenda kupokea

"maisha marefu Rebecca"
"maisha marefu mama Theresia" "happy birthday mama Leti njoo uzime mshumaa na kukata keki tufungue hafla hii ndogo" kila mtu alinipongeza akiniita jina alilolizoea wengine langu na wengine la watoto wangu

"jamani asanteni sana kwa upendo wenu wa ajabu sana sina cha kuwalipa, keki nitakata lakini siwezi kukata peke yangu na kuzima mishumaa peke yangu bila mume wangu mpenzi ngoja nimuite tufungue shughuli hii yaani

mmenishtua sana sijategemea" niliongea nikijawa na furaha wakapiga makofi na vigeregere hasa Margreth ambae alionekana kama ndiye mpambe mkuu, nikawaacha sebuleni na kurudi chumbani kumuita mume wangu

"vipi umeipenda hiyo zawadi?" nilimsikia mume wangu akiongea na simu kwa sauti ya chini
"mume wangu" nilimwita akashtuka na kunitazama
"ngoja" alimjibu aliyekuwa anaongea nae na kukata simu
"nakuhitaji sebuleni"
"ooh kula keki eeh?"
"kuzima mishumaa na kukata"
"sawa tangulia nakuja"
"hamna nataka tuongozane"

"basi twende mke wangu" alinijibu akiibeba simu yake
"simu si ungeiacha tu mume wangu?" "nataka nichukue matukio" aliniambia tukatoka wote mpaka sebuleni na moja kwa moja kwenye keki tukazima mishumaa na kukata na kulishana na kuwalisha kila mtu na nikashangaa mdogo wangu Diana hajaja tangu mambo yote yanaendelea hata kutoka chumbani hajatoka ikabidi niingie chumbani kwake nikamkuta amelala kitandani siyo usingizi ila yuko bize na simu yake

"Diana upo sawa?"
"dada uuwiii" alinijibu akijinyoosha nyoosha
"mbona hauji sebuleni?"

"naumwa dada yaani kiuno chote hapa hakina kazi na mgongo pia unawaka moto natamani kuinuka kuja lakini nguvu sina usinione bize na simu kuna assignment za chuoni hapa nafanya hapa kwa kujilazimisha maana laptop nimemuazima rafiki yangu sijarudi nayo"

"pole basi ngoja nikuletee keki" "usijisumbue dada nitakula na chakula baadae"
"sawa" niliitikia kiunyonge na kuanza kutoka chumbani kwake lakini nilipoufungua mlango ili kutoka

"dada!" aliniita nikageuka "abee??!!"
"happy birthday to you!"

"asante mdogo wangu" nilitabasamu nae akatabasamu kisha nikatoka chumbani kwake taratibu nikamkuta mume wangu Dawson amekaa kwenye kochi akiwa bize na simu nikamfuata na kukaa karibu yake akiwa hajaniona, nilipomgusa akashtuka

"ooh mke wangu ulienda wapi?" "mbona simu tu bize muda wote mme wangu?"
"kuna mambo ya kazini hapa hayajakaa sawa ndo nayaweka weka sawa mke wangu"

"ndo maana nilikwambia iache simu tu chumbani kwa sababu itakuchanganya leo huoni ni siku yangu ya furaha mume wangu jamani wewe bize na simu tu bize na simu?" nililalamika

lakini tukiongea kwa kunong'ona watu wasije wakatusikia

"usijali mke wangu halafu nina zawadi yako!" aliniambia akaweka simu yake mfukoni akainuka kwenye sofa la watu wawili tulilokuwa tumekaa yeye akaenda chumbani, muziki wa taratibu ukiwa umefunguliwa watu wakinywa soda na vitafunwa vingine

"oooopppss mbona simuelewi elewi huyu mwanaume sikuhizi??" nilijiuliza kimoyomoyo huku nikishusha pumzi ndefu na nikageuka na ndipo nilipokutana na simu yake aliyodhani ameiweka mfukoni kwenye suruali aliyovaa na kumbe haikuingia iliponyoka, nikaishika na kuitazama na ndipo niliposhtukia napokonywa na

mtu simu haraka haraka yaani kama naporwa na kutazama alikuwa ni mume wangu ambae sikujua hata amerudije rudije ndani ya sekunde chache hivyo nikabaki nimetoa macho....

*SEHEMU YA 04*

"mume wangu ndonini kuninyang'anya simu kama mwizi mbele za watu??" nilimwuliza kwa sauti ya chini

"supriseeeeee!!" aliongea kwa sauti na kunionyesha boksi lililofungwa vizuri kwa karatasi ya zawadi, boksi dogodogo

"nini hiki?"

"fungua mwenyewe uone" aliniambia watu wote wakasogea na kutuzunguka wakiwa na shauku ya kujua ni zawadi gani hiyo ninayopewa na mume wangu, nami nikafungua kijiboksi hicho kidogo kwa mbwembwe zote, kuwaonyesha kuwa mume ninae wenye wivu wajinyonge, nikakutana na simu nzuri aina ya Infinix mpya

"waaaoh asante mume wangu mpenzi" nilimwambia na kumkumbatia kwa furaha watu wote wakipiga makofi kunipongeza na kuniimbia wimbo wa 'Happy Birthday To You'

"uachane na Tekno sasa mke wangu karibu katika ulimwengu mwingine" aliniambia
"nakupenda mume wangu asante"

"asante usijali" alinijibu akinipiga piga mgongoni kisha wakati huo nikamwona mdogo wangu Diana akiwa amesimama kwenye mlango wa chumbani kwake akitazama kinachoendelea, mume wangu akanitoa nikiwa bado nina shauku ya kubaki kifuani mwake

"kwa niaba ya dada mwenye mdogo wake naomba kumlisha keki mdogo wa mke wangu na shemeji yangu mpendwa, Diana ambae hakuwepo wakati tunaendelea na matukio mengine" mume wangu akapiga makofi nami nikapiga makofi, Diana akasogea taratibu, mume wangu akachoma kipande cha keki, akakiacha cha kwanza cha pili na cha tatu akakichagua cha nne kikubwa kikubwa na kumlisha mdogo wangu kisha

akamkumbatia na kumpiga piga mgongoni

"asante shem" Diana aliongea
"karibu sana shemeji" mume wangu alimjibu wakiwa bado wamekumbatiana kwa sekunde kadhaa kisha Diana akaja na kunikumbatia mimi

"happy birthday dada"
"asante mdogo wangu" nilimjibu tukaachana kisha akarejea tena chumbani kwake nami nikabaki naitazama simu yangu

"haya sasa ni zamu ya wapendanao kucheza muziki pamoja wawili" Magreth aliwafurahisha watu na

kuwafanya waangue kicheko akijifanya kama Mshereheshaji (MC) na kweli muziki ukafunguliwa wa taratibu,

"cheza nae! cheza nae!!" wote walituhamasisha wakimaanisha mimi nicheze na mume wangu nikawa namtazama naona aibu kucheza mbele ya watu, mume wangu akanishika mkono na kunivuta karibu yake akanishika mikono na kuanza kucheza namimi

"mshike kiuno shemeji usiogope mkeo huyo, wenye wivu wajinyongageeee wakafie huko mbele kwa mbele inahu......." Magreth aliendelea kugongelea msumari watu wote wakicheka

"we kuna watoto" wengine walimkatalia
"kwani jamani si wanacheza tu muziki kwani nani amesema kucheza wapendanao ni siku ya harusi tu mimi mwenyewe mpaka leo nacheza na baba chanja wangu akikataa namrukia mgongoni" Magreth rafiki yangu ni muongeaji sana aliwafanya watu wacheke mpaka wengine soda zikawatokea puani, wengine wakapaliwa vitafunwa sambusa na soseji walizokuwa wakila na kunywa, nami nikajikuta nacheka, Diana alikuwa ametoka tena amekaa na mwanangu mdogo Leticia huku akituangalia, nilimshuhudia Leticia mtoto wangu mdogo akimwita mama mdogo wake huyo akitaka amvue viatu vilivyokuwa vinambana miguuni bila mafanikio,

wala Diana hakumtazama alikuwa macho yote anatutazama sisi, na ndipo mtoto alipomtikisa mama mdogo wake huyo kwa upendo lakini akageukiwa na mama yake huyo mdogo kwa hasira na kutimuliwa, akaondoka kwa unyonge kwenda kwa dada yake, Theresia, yote niliyashuhudia lakini sikutaka kuingilia kwa sababu huenda Diana kwa sababu ya kuumwa kama alivyosema alikuwa hataki usumbufu wa watoto

Muziki uliendelea, watoto walifukuzwa nje wakaenda kucheza na watoto wenzao wageni waliokuja na mama zao na baba zao, hasa wa majirani, wakipewa juisi na biskuti, ndani muziki ukawa unaendelea na mdogo wangu Diana akamuona mlinzi wetu wa getini aitwae Dully akamfuata

na kuongea nae huku mimi na mume wangu tukiendelea kucheza na watu wengine, tukamwona Diana akicheza na kijana huyo na yeye huku akituangalia sisi na kutabasamu, mume wangu aligeuza uso na kuniangalia mimi

"imetosha mke wangu nimechoka" "sawa mume wangu" nilimjibu tukaachana na kukaa

"bibi harusi na bwana harusi wetu wameacha kucheza lakini haimaanishi wageni waalikwa tuache kuserebuka endelea kuserebuka tu" Magreth alipambiza, akina mama wengine walishikana wawili wawili wakicheza kwa sababu ni wachache tu

waliofuatana na waume zao, wanaume walikuwa watatu tu

Tulikaa na mume wangu ambae alishika chupa yake ya soda na kuanza kunywa taratibu lakini akiwaangalia sana Diana na yule kijana mlinzi wetu, Dully aliyekuwa akicheza nae

"unamwangalia sana shemeji yako ataacha kucheza bure"
"akiacha kaamua tu siyo kwa sababu yangu" alinijibu akainuka

"unaenda wapi?"
"kuongea na simu mara moja" alinijibu na kuongea na simu humu ndani kelele, aliniambia nikatikisa kichwa na moja kwa moja akatoka na alipopita karibu na mdogo wangu Diana na yule mlinzi

Dully, nikaona akimnong'oneza yule kijana, wakaongozana wote wawili kuelekea nje, Diana akabaki amesimama peke yake

Magreth rafiki yangu akanifuata na kuninong'oneza sikioni

"tunaweza kuongea wawili mimi nawewe?"
"bila shaka"
"nakuomba nje nifuate" aliniambia akitangulia nami nikainuka kumfuata lakini yeye akaitwa na mama mmoja, mimi nikatoka mwenyewe mpaka barazani wakati nikiwa nakata kona nikasikia watu wanazungumza kwa kunong'ona ikabidi nichungulie

"samahani bosi aliniomba tu nicheze nae muziki sina mahusiano nae yoyote" Dully alikuwa akiomba msamaha kwa mume wangu

"amekuomba mwenyewe mcheze ndo unamshika kiuno vile, huwezi kucheza nae mbalimbali mpaka umshike shike, hujui kama yule ni shemeji yangu nawajibika kwake kwa lolote linaloendelea akiwa ndani ya nyumba yangu??"

"mimi sikutaka kumgusa alisema Dully mbona unaniogopa ogopa nishike kama dada walivyoshikana na shemeji yangu, samahani bosi najua kama ni shemeji yako na tunaheshimiana sana mimi na yeye sikuhizi samahani"

"nikikuona tena karibu na shemeji yangu Diana unajisogeza sogeza na kung'ata ng'ata maneno nitakuumiza na kazi itakuwa basi sijui umenielewa???!!!" mume wangu alikuwa mkali sijawahi kuona mpaka kijana wa watu akabaki anatetemeka,

"ukali huu wote wa nini mume wangu mbona jambo dogo lile??" nikabaki nimeshangaa....

*SEHEMU YA 05*

Nilimshangaa mno mume wangu Dawson, kwanini amgombeze kiasi hicho mlinzi Dully kisa tu eti alikuwa anacheza muziki na shemeji yake yaani

mdogo wangu Diana, tena alikuwa amekasirika haswa siyo wa utani utani

"nenda kaendelee na majukumu yako" "sawa bosi!" Dully alijibu akiivua kofia 'capello' yake kichwani aliyoiona nzito kutokana na kufokewa na bosi huyo yaani mume wangu akaanza kuondoka taratibu kuelekea getini na soda yake mkononi nami wakati nikitaka kugeuka nirudi nyuma mume wangu asinione kama nilikuwa nasikiliza maongezi yao nikashtukia maji mengi yananimwagikia mwilini nikashtuka na kugeuka mzima mzima, nikaongezewa maji mengine na kuloweshwa mwili mzima kama ningekuwa nimeshika simu mkononi basi ingeingia maji lakini kwa bahati nzuri sikuwa na simu mkononi

"jamaniiii ndo nini??!!" nililalamika nikijifuta futa maji mwilini
"happy birthday to you, happy birthday to you happy birthday dear Rebeccah happy birthday to you!" niliimbiwa wimbo na kupigiwa makofi nilipojifuta maji usoni na kutazama nikakutana na wanakwaya wenzangu waliokuwa wamefuatana na mama mchungaji kutoka kanisa ninalosali

"jamani jamani ndo nini kunisupprise kiasi hiki jamani nimefanya jambo gani kubwa uuuwiii!" nilifurahi kuwaona nikiruka ruka

"kazi ya Magreth hiyo sisi tulikuwa wala hatujui kama ni siku yako ya kuzaliwa leo" mama mchungaji

aliongea wakiwa ndo wameingia kwangu muda huo

"bora useme wewe mama mchungaji maana nikisema mimi mwenyewe kujisifia Rebecca ataniona kama ninapenda sifa na najifagilia saaaanaaa" Magreth kama kawaida yake

"asante Magreth jamani dah nimefurahi kuwaona, karibuni ndani karibuni pia nimeandaa chakula kwanza kuna vitafunwa ngoja mimi nikabadilishe nguo nimelowana hatari mama mchungaji karibu ndani"

"ngoja nikuongeze ndoo nyingine ya maji nimalize uchu wangu wa kumuogesha mtoto wa mwanamke

mwenzangu ili ukibadili nguo basi nisipate tabu ya kukutamani tena" Magreth alijibu akiinua ndoo animwagie maji tena

"eeh Magreth basi imetosha kha" mama mchungaji alimzuia
"asante mama mchungaji maana nimepaniwa kweli na huyu mwanamke bora unitetee" nilijibu tukicheka na kufurahi, nikaelekea moja kwa moja chumbani kwangu kubadilisha nguo na hazikuzidi hata dakika mbili mume wangu aliingia chumbani

"mume wangu Dully mbona kama nilikuona unamgombeza pale kulikoni?"

"niwewe uliyekuwa unatuchungulia kumbe?"
"wala sikuwa nawachungulia ila tu niliwaona"

"nilikuwa namuonya mambo fulani fulani naona ameanza tabia za uhuni uhuni humu ndani kwangu namimi sipendi uhuni"

"uhuni gani tena?"
"mimi nikafikiri ulinisikia wakati namgombeza mbona unaniuliza maswali mengi tena?" aliniuliza akihangaika kutafuta shati

"unatafuta nini kwani mume wangu?" "shati"
"unatoka kwani?"

"nimepigiwa simu ofisini kuna tatizo tunatakiwa tukalitatue usiku mzima wa leo"
"mh mume wangu mbona matatizo matatizo na vikao vya dharura vingi sana ofisini sikuhizi kuna shida gani?" "bosi mpya kaja amekuja na mfumo wake anatuendesha endesha tu atakavyo"

"pole mume wangu shati hili hapa vaa kwahiyo utarudi usiku sana?" "hapana kesho asubuhi"
"mh mme wangu asubuhi tena?"

"yap" alinijibu huku akiendelea kutafuta shati wakati nimeshalishika mkononi shati nimemwonyesha

"baby shati si hili hapa?"

"hapana kuna shati nalitaka hili hapa" alilipata shati jekundu
"mbona shati hilo hujawahi kulivaa ofisini hata siku moja na siyo shati la kazini limekaa tu kimtoko mtoko?"

"usiku saa hizi huyo mtu atakaeacha majukumu yake ya kazi akaanza kulitazama shati nililolivaa ofisini atakuwa na lake jambo"

"mh haya ngoja nikupasie!" nililichukua na kumpigia pasi haraka haraka akalivaa na kujipulizia pafyumu maana hakuoga tena,

"kesho, utaniagia kwa wageni" "sawa baby umesahau kitu!"

"kitu gani?" aliniuliza nikamwonyesha ishara anibusu shavuni, akanibusu haraka haraka

"asante namimi je?" nilimwuliza nikimshika mkono alipotaka kuondoka, akatega shavu lake nikambusu mashavu yote mawili na kwenye paji la uso

"asante!"
"Mungu akulinde" nilimwambia akatikisa kichwa na kuondoka, nikamsindikiza mpaka barazani akaingia ndani ya gari, mlinzi akamfungulia geti akaondoka ikiwa ni mida ya saa moja moja giza limeshaingia

"bwana mkubwa anaenda wapi tena?" kumbe Magreth alikuwa nyuma yangu amembeba mtoto wangu mdogo, Leticia

"amepata dharura ofisini"
"ohoo sawa, vipi umemwona mchungaji Mbaga?" alitikisa kichwa

"kwani amekuja, nimemwona mama mchungaji tu"
"eeh amekuja na kwaya sema alikuwa anaongea na simu muda ule nje kule kamsalimie" Magreth aliniambia nikafuatana nae haraka haraka mpaka ndani na kwenda kupiga goti mbele ya mchungaji huyo kiongozi wa kiroho wa kanisa ninalosali

"bwana asifiwe baba"

"amen za uzima"
"njema shikamoo baba"
"marahaba hongera kwa kutimiza mwaka mwingine"
"asante baba"
"Mungu akakupe miaka tele ya uzima, afya, amani na baraka nyingi wewe na familia yako!"
"amen baba asante kwa maneno ya baraka napokea"
"lakini kuna ndoto nimeota siyo nzuri juu yako mwanangu imenitia hofu, usiku mzima nilikosa amani"

"ndoto gani baba?" niliingiwa na wasiwasi

"mume wangu twende tuwahi kwenye mkesha wa jimbo muda unaenda" mama mchungaji aliingilia maongezi

yetu akiwa amebeba pochi yake akimuita mumewe huyo

"haya mwanangu ngoja tuwahi kwenye mkesha tunashukuru kwa soda na vitafunwa"
"mngesubiri basi baba niwaandalie chakula na mama mule kabisa?"

"hapana mwanangu huko tunapoenda tumeandaliwa chakula sasa tukishiba hapa tutashindwa kula cha huko, watatushangaa tukiacha chakula chao wakati wameshatupa taarifa kuwa wametuandalia uwe na amani hapa ni nyumbani kwetu siku yoyote tutapiga simu tutasema tunakuja kula na kunywa tutengenezee kitimoto ile"

"hahahaha baba mchungaji kwa kitimoto tu" nilicheka
"yaani huyu baba yako kwa wiki bila kuitafuta hiyo nyama anahisi kama wiki haijapendeza!" mama mchungaji aliongea akimshika mumewe huyo ambae mguu mmoja alikuwa anachechemea (aliumia kwenye ajali ya pikipiki siku za nyuma)

"nitawaandalia na kuwaita baba na mama hicho kitoweo muje kula na kunywa munipe mibaraka nijichotee mpaka imwagike"

"yaani utakuwa umefanya la maana" mama mchungaji aliongezea tukacheka nikawasindikiza mpaka nje na kuwalipia bodaboda kila mtu ya kwake iwapeleke stendi na nikampa mama mchungaji

hela ya taksi kimya kimya bila mchungaji kujua maana angekataa tukaagana wakaondoka nami nikarejea ndani

"ndoto gani hiyo mchungaji aliyoiota mbaya ya kunihusu??" nilijiuliza huku nikijikuna kichwa....

INAENDELEA!

More Products On Discount
More Products From This Seller
Best Sellers List
Best Seller
10,000 Tsh.
(5.4)

Sold by: Gaston Ngailo

Best Seller
10,000 Tsh.
(69.8)

Sold by: Samuel Macha

Best Seller
10,000 Tsh.

Sold by: PASTOR TONY OSBORN

Best Seller
3,000 Tsh.
(16.4)

Sold by: ABDULKADIR MASSA

Best Seller
10,000 Tsh.

Sold by: PETER TARIMO

GetValue Recommendations
Old is Gold