Moyo Wa Baba: Tabia Halisi Ya Mungu Ambayo Wengi Hawaijui
Uchambuzi wa Kimaandiko juu ya Tabia halisi ya Mungu
Si ajabu leo ukakutana na watu ukawauliza kama wanamjua Mungu wakakujibu ndiyo hadi pale utakapomuuliza zaidi, yukoje, ana tabia gani n.k halafu bado usipate jibu. Kujua kwamba Mungu yupo ni jambo moja, lakini kujua tabia yake ni jambo lingine. Lakini, Je, Mungu anafananaje? Kama ni roho nitajuaje tabia zake, nitajuaje mapenzi yake? Mungu amejifunuaje? Si ajabu leo kuwakuta wakristo wakisema “Kumjua Mungu ni jambo gumu sana” hata wengine hudiriki kusema “Mambo ya Mungu hayaelezeki” kama mimi nilivyokuwa naamini. Hii inawafanya wakristo waishi maisha ya kubahatisha tabia halisi ya Mungu na hivyo kubaki kwenye uhusiano wa mashaka na Mungu na imani isiyo na msingi imara.
Lengo la kitabu hiki ni kukufunulia na kuchambua moyo au tabia halisi ya Mungu kwa namna ambayo itafukuza giza lote ndani yako na kukuacha huru katika mahusiano yaliyojengwa na taarifa sahihi juu ya Mungu.