
MIZIMU YA UKOO FAMILY SPIRITS NA NAMNA YA KUOMBA ILI UTOKE
Kila UKOO au familia huwa kuna tatizo linalowapata watu wengi mfano kuna familia moja mabinti wengi huwa wanakuwa wajane familia zingine kuachika, wengine umaskini, roho hizi za mizimu ndio huwa zinasababisha matatizo hayo
MIZIMU YA UKOO
{FAMILY SPIRITS}
Mizimu ya ukoo ni roho za kishetani zinazotawala ukoo au familia Fulani
Karibu kila ukoo una maagano yaliyowekwa ama kwa kujua au kwa kutokujua wanachokifanya.
Katika ulimwengu wa roho, shetani hawezi kummiliki mwanadanu mpaka kuwe na maagano maalum aliyoyaweka mtu huyo; wengine wanasainishwa mikataba katika ndoto, wengine wakati wa kuzaliwa, wengine hukuta maagano yamekwisha kufungwa na wazee waliopita katika ukoo au familia husika, na wengine mimba inapotungwa.
Roho hizi za ukoo ndizo zinazosababisha nira na vifungo katika ukoo fulani. “nitawaendea watu wakubwa, nami nitasema nao; kwa maana hao wanaijua njia ya BWANA, na hukumu ya Mungu wao. Bali hawa kwa nia moja wameivunja nira na kuvikata vifungo.” Yeremia 5:5
Hapa anaposema habari ya watu wakubwa, ni wale ambao baada ya kuokoka wamevunja nira na vifungo vya mizimu ya koo zao. Kwa maana hiyo kumbe katika kanisa wapo watu wakubwa na watu wadogo.
Watu wadogo.
Hawa ni wale ambao wameokoka lakini hawafanyi chochote ili kujiondoa katika nira na vifungo. Hawa utakuta huduma zao zimefungwa, nguvu ya Mungu inakuja na kuondoka, uchumi umefungwa, afya zimefungwa hata mahusiano pia yamefungwa.
Watu wakubwa.
Hawa ni wale ambao wameokoka na wakapata neema yaa kuvunja nira na vifungo vya Ibilisi. Hawa ni wachache sana katika kanisa, na kanisa huwa linawategemea sana, kwa maana wana nguvu ya Mungu ya kudumu. Hata kama bado ni maskini, utakuta tayari anaonesha dalili za kuinuliwa sana. Hawa huwa hawateswi sana na roho za magonjwa.
Mungu amesema, tuvunje kila nira “…..kuwaacha huru walioonewa, na kwamba mvunje kila nira? ” Isaya 58:6
Mizimu ya ukoo ndio inayosababisha laana za ukoo, kwa mfano; ukoo Fulani unakuwa maskini sana, magonjwa ya kufanana kwenye ukoo, hasira, kukata tamaa, kufa mapema na mengine mengi. Bwana amesema anawapatiliza wana maovu ya baba zao mpaka kizazi cha tatu na cha nne. “……kwakuwa mimi, BWANA, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao” Kutoka 20:5.
Neno la Mungu linasema, “ Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.” 2 Wakorintho 5:17 Kwa mujibu wa neno hili tunatarajia kuona mabadiriko makubwa sana ya kimwili na kiroho kwa mtu yeyote anayepiga hatua kumkabidhi Yesu maisha yake. Lakini kwa sababu ya vifungo vya mizimu ya ukoo wakristo wengi leo wako makanisani, bila mabadiriko yoyote, ukoo wao hauzai, na yeye utakuta ameokoka na anaombea watoto na bila mafanikio, ukoo wake ni maskini; na yeye ana umaskini wa kutupwa. Wakristo wengi wanafanya kazi ya Mungu huku hawana upako, kazi yenyewe inakuwa ngumu kwao; wengi wanaacha utumishi na kurudi kwenye shughuli zao za kawaida. Ndio maana makanisa mengi yanafunguliwa na yanasambaratika na utakuta watumishi hawana la kufanya na wamekata tamaa wanaombea watu lakini hawafunguliwi.