Sura ya Kwanza: Safari ya Maisha.
Sura ya kwanza imezungumzia kuhusu safari ya maisha kuanzia tunavyozaliwa, malezi na makuzi yetu ya kuanzia utoto, ujana hadi utu uzima, changamoto mbalimbali tunazokutana nazo katika safari hiyo tukiwa wadogo mpaka kuingia shuleni na uhalisia wa mpaka tunapofika chuo na kisha kuingia mtaani na uhalisia wa maisha ya mtaani na ajira, jinsi ya kukabili changamoto na kutengeneza uhai mpya wa mafanikio, namna ya kujenga imani na kumtumainia Mungu hadi kujenga jukwaa jipya la kifursa na kujitegemea mtaani, kuongeza maarifa na kujielewa zaidi kama kijana.
Lakini pia kimegusia jinsi mfumo wa makuzi na mataba yanavyotengenezwa katika maisha, jinsi gani tabaka la juu la wanaofanikiwa wanavyowaza katika hatua tofauti na tabaka la maisha ya kawaida ya chini.
Sura hii inawafaa zaidi vijana, watoto, lakini pia wazazi na walezi wanaowalea na kuwakuza watoto wao, ila pia wale wote wanaopambana katika safari ya maisha lakini hawaoni tumaini, hakika ni tiba na uponyaji kwako mpambanaji katika safari hii ya maisha.
Baada ya kusoma utakuwa ni mtu mpya mwenye mtazamo chanya na wa tofauti kabisa kuelekea ngazi mpya ya tumaini na mafanikio maishani.
Sura ya Pili: Jukwaa, Ndoto na Maamuzi.
Sura hii imezungumzia kuhusu mawazo ya ndoto zetu kimaisha, changamoto mbalimbali na jinsi tunavyozikabili, lakini pia hamasa na uchukuaji hatua wa maamuzi sahihi katika maisha na ndoto zetu hizo, pia falsafa za kimaisha na watu tunaokumbana nao katika safari ya kutimiza ndoto zetu hizo ili kuweza kuendelea na safari kwa amani na tija.
Sura ya Tatu: Mawazo Hayaji Yakiwa Yamekamilika.
Sura hii inazungumzia kuhusu kuanzisha kitu ama jambo hata kama bado haujawa na picha kamili ama kujipanga vya kutosha, ni kwa namna gani mambo yanavyokaa sawa kadri unavyosonga mbele kwa imani na uwajibikaji, pia ndoto zako na umuhimu wako katika kutimiza ndoto zako hizo na juwa tija kwa jamii.
Sura ya Nne: Nyakati, Vikwazo, Mtazamo Mpya na Kusudio Lako.
Sura hii imezungumzia kuhusu namna mtazamo wako na mabadiliko ya fikra na mwenendo vinavyoweza kuathiri maisha yako katika mtazamo chanya ama hasi, maono, vikwazo na pia nyakati mbalimbali na falsafa anazopitia mwanadamu katika safari yake ya mabadiliko, pia kuleta hamasa na kutia moyo kwa kutoa mifano mbali mbali ya watu waliofanikiwa katika maisha wakiwa wameshafika umri mkubwa na katika mazingira yenye changamoto, hivyo kutupatia jibu kuwa umri ni namba tu na usikate tamaa muda wowote unaweza kuibuka mshindi wa mafanikio katika maisha na kutimiza kusudi la ndoto zako. Ni kitivo kilichosheheni maarifa makini ya kimaisha.
Sura ya Tano: Kutoka 57.
Sura hii inazungumzia safari ya maisha, changamoto mbalimbali, kutokata tamaa haijalishi upo wakati gani wa maisha.
Sura ya Sita: Maisha Yana Sura Mbili.
Sura hii inazungumzia kuwa, maisha ni mchanganyiko wa mambo na hisia, usimdharau mtu, mthamini kila mmoja, jiamini na jithamini pia, kila mmoja ana safari yake na alichokusudiwa na Mungu.
Sura ya Saba: Watu Wanaokuja Maishani.
Sura hii imezungumzia kuhusu aina mbalimbali za watu mbalimbali wanaokuja katika maisha yetu wakiwemo marafiki katika maisha, nia na madhumuni yao, athari zao na namna ya kuwatambua na kujiepusha ama kuwa na mipaka na kujikinga nao katika maisha.
Si kila umuonae maishani yupo karibu na wewe na anakuchekea usoni basi ana nia njema na tabasamu la kweli nawe kutoka moyoni, dunia imejaa usaliti na unafiki, watu wa kweli na dhati ni wachache kwako katika maisha haya; ishi kwa umakini.
Sura ya Nane: Ubongo / Akili na Utashi.
Sura hii imezungumzia zaidi kuhusu namna mwanadamu alivyo nadhifu katika kutatua changamoto mbalimbali, kuleta maendeleo na kufanya mabadiliko ya aina yake tofauti na wanyama wengine endapo akitumia akili zake vyema na kwa ufasaha.
Inatukumbusha kuwa, nyenzo kuu tuliyonayo wanadamu ni ubongo wetu wenye akili iliyo nadhifu ingawa tunaweza kuwa hatuna nguvu, ukubwa na kasi kama wanyama wengineo walivyo msituni, ila sisi ni zaidi ya hao viumbe endapo tukijitambua kuwa nyenzo pekee kuu ni akili tuliyobarikia na Mungu na endapo tutaitumia kwa usahihi.
Sura ya Tisa: Uongozi / Nguvu ya mwenendo.
Hii ni sura inayozungumzia sifa za kiongozi bora, maadili, changamoto, athari za utawala na matumizi ya mamlaka, jinsi gani kiongozi anatakiwa aenende na kuwa. Ila pia kutoa hamasa na ujasiri kwa kiongozi na mtawala katika utawala na himaya yake.
Sura hii inawahusu zaidi wanasiasa, wazazi na walezi, lakini pia vijana wanaojiandaa kuja kushika hatamu mbalimbali, na inaanzia kuanzia ngazi ya familia, kaya, jamii, taifa hadi dunia kwa ujumla.
Pia imetumia mifano ya viumbe kama simba na tai katika himaya zao katika kuelezea taswira halisi ya uongozi na utawala.
Sura ya Kumi: Wazazi.
Kama tujuavyo milango ya baraka na laana katika maisha ipo mikononi mwa wazazi wetu, ni watu muhimu sana katika uhai na maisha yetu, ndio mabawa yetu Mungu huwatumia kama mlango na nyenzo ya kutuvusha katika vilinge mbalimbali katika maisha, hivyo ni viumbe muhimu sana katika maisha yetu. Jamii ama taifa pasipo wazazi ni sawa na chombo cha usafiri kisicho na dereva salama.
Sura hii imezungumzia nini maana ya wazazi, umuhimu wao kwetu katika baraka na laana za maisha yetu, umuhimu na namna ya kuwaheshimu, kuwatunza, kuwa faraja katika maisha katika kutekeleza ibada na kulwta baraka za maisha.
Sura hii inawafaa zaidi vijana ambao hupaswa kujua umuhimu wa wazazi, lakini pia kwa wazazi wanaowaandaa watoto walio taifa la kesho na pia watoto ambao hutakiwa kukua katika misingi ya kujua umuhimu na maana ya wazazi mapema ili kujenga kizazi chenye nidhamu katika maisha.
Sura ya Kumi na Moja: Dondoo za Ndoa na Mahusiano.
Hii ni sura inayozungumzia mambo mbalimbali kuhusu mahusiano na ndoa, changamoto zake na mambo mbalimbali katika kukabili na kudumisha mahusiano mema, lakini pia kutoa taswira kwa wale wanaotarajia kuingia katika swala hilo nyeti.
Sura ya Kumi na Mbili: Imani na Muumba.
Hii ni sura inayozungumzia asili yetu na chanzo cha kila kilichoumbwa duniani, lakini pia inazungumzia kuhusu uwepo wa Mungu na namna gani mwanadamu kwa dhamira yake mbovu anavyotaka kuharibu utukufu na kusudio la Mungu hapa duniani na kuleta utengano na maharibifu.
Sura ya Kumi na Tatu: Kusudi la Mungu Kwako.
Sura hii inazungumzia dhumuni la sisi kuwepo hapa duniani, je Mungu alituumba na kutuweka kwa makusidio gani? Na je ni mambo gani yanaweza kutengeneza na pia kuharibu kusudio hilo na ndoto zako za kuwa hapa ulimwenguni.
Sura ya Kumi na Nne: Ulimwengu wa Kanuni na Sheria.
Hii ni sura inayozungumzia zaidi kuhusu kanuni, sheria na taratibu mbalimbali za kimaisha, lakini pia dondoo za falsafa mbalimbali muhimu za kimaisha.
Sura ya Kumi na Tano: Jicho la Kijasiriamali.
Hii ni sura inayohusu jukwaa la kijasiriamali, biashara, pia tofauti kati ya kuajiriwa na kujiajiri, athari na mafanikio yake, changamoto mbalimbali na maandalizi ya hapo baadae hata baada ajira kufika ukomo, lakini pia mawazo mbalimbali ya kibiashara ikiwamo utengenezaji wa sabuni ya maji.