MAAJABU YA KUWEKA AKIBA
Jinsi Tabia Ya Kuweka Akiba Inavyoweza Kukufanya Tajiri
Tangu umezaliwa mpaka
leo hii, ni unaposhika kitabu hiki mikononi mwako ni wazi kuwa fedha nyingi
tayari zimepita mikononi mwako. Hivi laiti ungekuwa umeweka utaratibu wa kuwa
unatoa kiasi kidogo kwenye kile ambacho unapokea na kukiweka kama akiba,
unadhani leo hii ungekuwa na kiasi gani?
Niliwahi kumwuliza dada
mmoja swali hili hapa, akawa amefikiri kwa muda, kisha akaniambia, “Loo!
Ningekuwa na fedha nyingi sana”. Bila shaka na wewe utakuwa na majibu kama hayo
ambayo huyo dada alikuwa nayo.
Kila mtu huwa anapokea
fedha kwa viwango tofauti, japo kiasi ambacho unapokea sasa hivi kinaweza
kuonekana kidogo. Lakini ukiweka utaratibu wa kuweka akiba kutoka kwenye hicho kidogo, ni wazi kuwa itafikia hatua ambapo
hicho kidogo kitakuwa kikubwa.
Ni imani yangu kuwa
baada ya kuwa umesoma kitabu hiki hapa, utachukuka hatua na kuanza kuweka akiba
bila ya kuchelewa. Nipo nafikiri tu kuwa kwa mfano, ukimfundisha mtoto wako
misingi ambayo utajifunza humu ni wazi kuwa mpaka anakuja kufikisha miaka 18 au
20 basi atakuwa ameweka akiba ya kutosha kumfanya hata aweze kujilipia ada ya
chuo kikuu bila kuhitaji mkopo wa chuo. Na kwa sababu atakuwa amejenga msingi
imara basi ni wazi kuwa bado kiasi zaidi kitakuwa kinazidi kuingia kwake.