Kiranga Komo
Ni kweli kwamba ni suala la demokrasia ya mapenzi kumpenda yule umpenda bila kutazama rika. Lakini je, hali halisi? Wakati nao?
Upo wakati moyo wa mtu hutamani visivyotamanika. Hapa kwa dhati unaaswa kuepuka sana kuangukia mtegoni kwa sababu ya moyo wako na kuamua kuziacha akili zako bila faida. Kitakukuta cha kutamausha!
Katika riwaya hii, japo si mara zote, Panga, kijana mtanashati, mwungwana wa mtaa, anajikuta akiingia katikati ya dimbwi refu la mapenzi na mtu aliyemzidi umri. Ndugu wakasema, rafiki na majirani pia lakini sio la kufa halijawahi kusikia dawa. Kwa Panga ikawe bahati yake? Thubutu! Dunia hajaiumba yeye!
Mwandishi ametumia mandhari ya Waswahili eneo la Kiwalani kueleza desturi za wakazi wa huko kwa kina sana!