Kiongozi Aliye Choka
Pengine moja ya eneo ambalo halizungumzwi sana ni kuhusu uchovu wa viongozi. Hii inachangiwa na dhana potofu ya kuwaona viongozi kama “wanadamu wasio wa kawaida” ambao kuchoka hakuwahusu. Lakini ukweli ni kwamba viongozi ni wanadamu wa kawaida ambao wanachoka, na pengine ndio wanaochoka kuliko wale wanaowaongoza. Uchovu ni kuchakaa kwa nguvu za kimwili, Kihisia, Kiakili na Kiroho kunakosababishwa na jitihada za muda mrefu. Ufahamu wa watu wengi juu ya uchovu upo zaidi katika eneo moja tu, la kuchoka kimwili. Kuna maeneo makuu manne ambayo uchovu huweza kumuathiri kiongozi katika maisha yake ya kila siku ya kumtumikia Mungu, kwa kupitia huduma mbalimbali anazofanya. Maeneo haya ni kimwili, kiakili, kihisia, na kiroho.
Tunaishi katika ulimwengu uliojaa viongozi waliochoka, mfumo wa maisha umepelekea kuwa na viongozi wa namna hii, na wengi hufa mapema kwa sababu ya kuchoka. Kutokana na shinikizo la maisha na kutaka kufanikiwa wengi huteketeza na kupoteza nguvu zao kwa kasi.
Majukumu ya kihuduma tunayofanya kila siku yananyonya na kuteketeza nguvu zetu (kimwili, kihisia, kiakili na kiroho) na kama hatuna maarifa ya kuzirejeza tutajikuta kwenye hali ya uchovu kisha kuteketea kabisa kwa nguvu. Hali hii itaathiri afya zetu, akili zetu,hisia na roho zetu pia.
Hali hii tunaweza kuifananisha na bonge la barafu, linapokuwa peke yake mlimani, madhara yake yanaweza yasionekane, lakini likiviringika kutoka mlimani ndipo matokeo/madhara yake yataonekana.