HISTORIA YA DR MWALUSAMBO
HISTORIA YA MAISHA NA UTUMISHI WA MCH. ZEPHANIAH ENOCK MWALUSAMBO
UTANGULIZI.
“Historia ya maisha ya Zephaniah Enock Mwalusambo” ni kitabu ambacho nimekiandika kuelezea maisha yangu tangu kuzaliwa, kuokoka kwangu, elimu yangu, ndoa yangu, wito wangu, huduma yangu, pamoja na changamoto mbalimbali nilizozipitia katika utumishi wangu. Haya yote ni katika kipindi cha miaka sitini na sita ya umri wangu; miaka arobaini na tatu ya huduma ya uchungaji; miaka thelathini na miwili ya ukatibu; na miaka ishirini na mitatu ya kuwa mwalimu wa Chuo cha Biblia; na miaka arobaini na miwili ya ndoa.
Katika kitabu hiki nimeeleza historia fupi ya mabadiliko ya kanisa kutoka PHA, PHAM na mwisho PHAMT; na kila mabadiliko yalipotokea, yalileta na changamoto ambazo kwa wengine ziliwasaidia, na wengine waliharibikiwa. Umuhimu wa mabadiliko ndio uliotufikisha hapa tulipo sasa.
Mungu ametuweka kila mtu ajifunze kwa mwingine. Nimejifunza mambo mengi kwa walionitangulia kimaisha na kihuduma, ijapokuwa hawakuandika mahali popote, lakini mengi yameandikwa ndani ya moyo wangu. Naamini kuwa wengine watajifunza kupitia kitabu hiki kwa yale niliyoyafanya vema, hata na yale niliyoyakosea.
Mungu akubariki unaposoma kitabu hiki!