Hatari Ya Kuchoka
Kitabu hiki, Hatari ya Kuchoka, kimeandikwa kutoka moyoni, kwa lengo la kuwapa waumini nguvu mpya, maarifa, na motisha ya kuendelea kumtumikia Mungu bila kuchoka, hata wanapokutana na changamoto mbalimbali za maisha. Nilianza utumishi wangu kwa nguvu kubwa na maono makubwa ya kuleta mabadiliko katika maisha ya watu. Lakini katika safari yangu kama mtumishi wa Mungu, nimepitia vipindi vya kuchoka, kuvunjika moyo, na kukosa msukumo wa kuendelea mbele.
Kitabu Hatari ya Kuchoka ni zao la safari yangu binafsi ya imani na huduma, safari iliyojaa changamoto nyingi, lakini pia ushindi wa ajabu kwa msaada wa Mungu. Kama mtumishi wa Mungu, nimepitia vipindi vya uchovu, si tu kimwili, bali hasa kiroho. Nimeona jinsi ambavyo uzito wa changamoto za maisha, majukumu ya huduma, na hali ngumu zinavyoweza kumpelekea mtu kukata tamaa na kuhisi kushindwa kuendelea mbele.
Moyo wangu ulibeba mzigo wa kuwatia moyo wenzangu, hasa wale ambao wamefika mahali pa kuhisi wameshindwa katika safari yao ya kumtumikia Mungu. Hivyo, niliamua kuandika kitabu hiki kama mwongozo wa kuwapa nguvu mpya na kuwakumbusha kuwa uchovu sio mwisho wa safari. Badala yake, ni fursa ya kumkimbilia Mungu kwa ajili ya upya wa nguvu na shauku.
Katika kitabu hiki, utapata maarifa na mafundisho yanayotokana na Neno la Mungu na mifano ya mashujaa wa imani waliozidi uchovu na kukutana na Mungu kwa undani zaidi. Wengine walifikia kiwango cha kukata tamaa, lakini Mungu aliwapa ujasiri wa kuendelea. Naam, hata mimi mwenyewe nilijikuta nikiwa nimechoka, lakini neema ya Mungu ilinitia nguvu na kunipa upya wa moyo wa kuendelea kumtumikia.
Naamini kuwa kitabu hiki kitakuwa msaada mkubwa kwa wewe ambaye unahisi umefika mwisho. Mungu hajakumaliza. Kuna zaidi ambayo Mungu anataka kufanya kupitia wewe, na nguvu za Bwana ni nyingi zaidi ya uchovu wako. Tunapomtegemea Yeye, tunapata nguvu mpya kila siku.
Kumbuka, safari yetu ya kiroho haitegemei uwezo wetu binafsi, bali inategemea nguvu za Mungu zisizo na kikomo. Ni maombi yangu kwamba kitabu hiki kitakutia moyo usimame tena, upige moyo konde, na kuendelea na huduma yako kwa Bwana.
Ubarikiwe,
Nabii PD Yohana