Fatinah
Price:
8,000 Tsh.
Vendor:
Added To Cart:
0
Added to shop:
Jun 18, 2021
Product Views:
3,305
Sample
Kama Kuna Njia Ya kuingia, Kuna Njia Ya Kutokea!
Hali ya anga ilikuwa tulivu kabisa, ni utulivu uliofanana na asubuhi ama jioni lakini sikumbuki vizuri yaani sifahamu ni wakati gani huo, kwa mbali tu nilisikia mingurumo ya vyombo vya moto kwa sababu barabara nayo ilikuwa mbali.
Kwa ufupi nyumba ninayoishi ilijitenga kidogo na mji lakini karibu na nyumba zingine. Kwa hiyo si kwamba nyumba niliyoishi ndio ilijitenga lakini ni mtaa ndio ulijitenga na mji. Sauti pekee nilizosikia ni za watoto wa nyumba za jirani wakicheza michezo yao ya kitoto na mara chache nikisikia sauti za watu wazima wakizungumza au kuwaita watoto wao majumbani. Mradi pilikapilika na kila mmoja na lake.
Ndio hali halisi niliyokuwa napitia, wakati wapo waliokuwa wakifurahia maisha kwa upande wangu ndani ya nyumba yangu kuukuu nilikuwa katika ulimwengu wa peke yangu kabisa. Ulimwengu mgeni nisiouzoea na hali ya kutouzoea ndio inayonipelekesha puta sasa, maisha yangu yalitengeneza sinema ambayo kama angalikuwapo mwongozaji mahiri yeyote na popote duniani akaiweka katika mfumo wa sanaa za maonyesho angejizolea sifa kedekede.
Nilitoka chini, nikapanda mpaka juu kabla sijashuhudia anguko la ghafla ndani ya kitendawili kizito, anguko la ajabu nisilofahamu msingi wake haswa mpaka wakati huu. Ni maanguko ya namna hii ambayo wengi wenye kushindwa kuhimili hisia za ndani huishia kujidhulumu nafsi ilimradi tu akili na nafsi zao zisishuhudie fedheha, dhihaka na kila aina ya aibu inayoambatana na maanguko yao.
Wakati tafakuri hizi zikipita kichwani mwangu nilikuwa ndio natoka kuyafungua macho baada ya kupoteza fahamu kwa masaa mengi nisiyokumbuka, si kwa kuzirai ama vinginevyo bali kwa kilevi kingi nilichobugia siku iliyopita kabla sijakata fahamu. Hata hivyo sina hakika kama ni siku iliyopita ama vinginevyo, sina kumbukumbu nzuri kutokana na masaibu yangu na aina ya maisha ninayoishi kwa sasa.
Pamoja na uchovu mwingi lakini njaa nayo haikuacha kuniandama, sikuwa na nguvu mwilini hivyo nikajikokota kuinuka angalau nilipatie chochote tumbo langu. Nikajiinua kwa tabu na kukaa kitako katika kingo za kitanda changu kidogo chenye ukubwa wa mita nne kwa pande zote, cha mbao. Nikamudu kuinuka na kuketi lakini bado nikafeli kusimama kwa mfululizo, maana kichwa kilipitiwa na kizunguzungu kidogo cha ghafla nikainamisha kichwa kiasi kisha kiganja changu cha mkono wa kulia kikavinjari maeneo yote ya kichwa. Nikafikicha macho kwa uchovu mwingi nisioelewa ni wa mawazo, njaa ama ulevi. Ulikuwa mchanganyiko wa kusikitisha tu ukinisulubu bila huruma katika ulimwengu huu dhalimu.
Mkono wangu wa kushoto ulikamata ukingo mmoja wa kitanda ili kupata uwiano sawa. Mkono wa kulia uliokuwa ukipapasa kichwani ndio ulibaini nywele zangu za kipilipili zilizojiotea bila busara, haraka fahamu zangu zikayaelekeza macho kujaribu kuvinjari maeneo yote ya mwili ambayo yangefika. Ni kwa mara ya kwanza nikabaini namna afya yangu ilivyozorota, nimedhoofu, vijana wa mjini wanasema ‘nimepoteza’. Nimeshapoteza ramani ya vita sasa natangatanga bila uelekeo.
Nikazikusanya nguvu na baada ya kujihakikishia sasa naweza kusimama basi nikanyanyuka, ukafuata mwayo mrefu kabla sijajinyoosha kuweka sawa mwili. Na kabla sijafanya lolote nikakumbuka sijashika simu yangu kwa muda mrefu, nikageuka nyuma na kutazama katika kona moja ya kitanda ambako nilitegemea ningeiona, kwa kawaida nina desturi kila ninapolala basi simu ningeiweka karibu na mto wa kulalia, yaani kichwani. hiyo nilikuwa napoteza kila kitu. Haikuwepo. Kichwa kikapata moto maana kwa kuipoteza simu
Nikarudisha shingo yangu mahali pake kama awali kisha nikafikicha uso wangu ambao hata hivyo bado haukupitishwa maji. Mbele yangu ukutani palikuwa na kioo kidogo nikakitazama kwa muda, taswira yangu iliyoonekana kupitia kwenye kioo ilinirudisha mbali sana kihisia, kabla sijakuwa Almasi huyu wa sasa. Nikapiga hatua chache kukisogelea kisha nikasimama mbele yake. Nilikuwa kifua wazi lakini chini nilivaa suruali ngumu aina ya jeans kwa maana kwamba nililala na suruali!
Mbele ya kioo nilikuwa natazamana na mimi mwenyewe. Nikatumia muda huo kujitathimini kupitia kioo hicho kuanzia utosini mpaka maeneo ya kifua ambako ndio mwisho wa urefu wa kioo hicho. Ama hakika kweli nilipoteza mwelekeo. Nilikaa mbele ya kioo kwa takribani dakika kumi bila kusemezana chochote na mimi wa kwenye kioo. Sifahamu ni kwa nini lakini nilijikuta nikiangusha tabasamu, ambalo kimsingi si la furaha wala matumaini bali lenye tafsiri ya ushindi ambao haijulikani lini utadhihirika. Ushindi kuhusu nini? Nashindana na nani? Sijui.
“Hii ni vita ya nafsi, vita mbaya sana isiyotajwa” nikajisemesha nikishusha pumzi ndefu bado nikiendelea kusalia mbele ya kioo nikipitisha kumbukumbu mbalimbali zilizokuwa zinakuja na kukata harakaharaka utadhani zinafanya hadaa na nafsi yangu pweke.
Kwa ufupi huyu niliyekuwa namtazama sasa sio mimi yule wa miezi kadhaa nyuma, na nilipokuwa nikiendelea kusimama mbele ya kioo nikasikia mlio wa simu yangu kutokea katika kona nyingine ya kitanda. Ilikuwa kwenye muito wa mtetemo.
"Mungu mkubwa!" nikajisemea kwa sauti ya chini maana niliamini simu nilishaipoteza ulevini kwa kuwa sikumbuki nilifika vipi nyumbani wala saa ngapi. Kumbe nilipotupia shati baada ya kuvua ndipo simu ilipokuwa, haraka nikapiga hatua kuifuata nikafunua shati, simu ilikuwa chini ikiendelea kuita.
Nikatazama mpigaji, alikuwa mama yangu, nguvu zikaniisha. Kwa makusudi matupu sikutaka kuipokea maana ni wiki sasa mfululizo anapiga sipokei sio kwa kupenda lakini ni kwa sababu angetaka kusikia kutoka kwangu shida ni nini na mimi siko tayari kumwambia. Fedheha inayonikabili sikuweza kuibeba.
Nilikuwa nikipambana kumalizana na kadhia inayonikabili ili wakati mwingine akipiga niwe tayari kuipokea nikiwa na majibu. Katikati ya hii fedheha inayoendelea sikuwa na chochote cha kumwambia na pengine akijua yale yaliyonipata huenda ingeharakisha kifo chake kutokana na mgogoro wa afya anaopitia pia. Sikutaka hili litokee wala sikutaka niwe chanzo cha kifo cha mama.
Nikaendelea kuitazama simu kwa kitambo ikiita tu mpaka ikakata, kabla sijairudisha mahala pake ikaanza kuita tena. Sikuipokea vilevile!!
Ilipokata nikabofya namba kadhaa kuipigia simu nyingine ikaita kidogo ikakatwa.....!!!
“Nimekwisha” nikajisemea.
Nikatoka ndani ya chumba changu taratibu na kujielekeza katika chumba kingine cha uani, hicho anaishi mwanadada mmoja mlalahoi mwenzangu ambaye riziki yake inategemea kudra za miguu yake kupitia biashara ndogondogo za kutembeza mitaani. Sabrina, huyu ndio alikuwa mkombozi wangu kila ninapokwama. Mara nyingi alipopika chakula basi huja kunigongea mlango ili tugawane umasikini. Na siku zote nilikataa kukwepa kumuongezea mzigo usio na tija lakini leo njaa ilinikamata penyewe, minyoo ya tumbo ilisakata rhumba vilivyo kwa hivyo sikuwa na namna zaidi ya kujisalimisha kwake!
Pupa zikaniisha nilipokutana na kufuli zito mlangoni kwake, hayupo. Alishajihimu mapema kabisa kuwahi mihangaikoni. Nikahisi vile nitakavyokiona cha mtema kuni siku ya leo, taratibu nikaketi kitako katika ngazi za mlango wake. Kama ni mwambo huu umetakata!
Naitwa Almasi Hobela.
****
M
ahali fulani jijini Dar Es Salaam, jiji lililosheheni raha na karaha, jiji ambalo watanzania wengi wanaotokea mikoa mingine ndoto zao ni kulikanyaga kwa namna iwayo yote, iwe kwa matembezi ama kwa shughuli mbalimbali. Naam jiji lililochangamka vya kutosha. Sura ya Tanzania.
Ni katika baa iliyofahamika kama Micasa Lounge maeneo ya Ubungo, napo mambo yalikuwa moto, Jumamosi hii palifurika mapema sana. Wateja mbalimbali walijazana mahali hapa wakizipatia roho zao kile zinataka kwa nafasi zao kulingana na matakwa. Wenye kushibisha matumbo yao walifanya hivyo na wale wenye kuhusudu vinywaji basi wangepata iwe vile baridi au vilevi ili mradi kila mmoja kwa wakati wake alijitahidi kufanya kile kilichomfikisha mahali hapo.
Bendi moja isiyo maarufu iliendelea kutumbuiza taratibu kwa kuiga nyimbo na mitindo maarufu na isiyo maarufu. Bendi hii japokuwa haikufahamika lakini ilijengwa na wanamuziki mahiri kweli waliofanikiwa kuzikonga nyoyo za wateja vilivyo. Mteja yeyote aliyeguswa na wimbo wowote angekwenda kuwatuza bila pingamizi ama aliyehitaji wimbo aupendao upigwe angeomba kwa dau dogo tu. Raha rahani.
Bado ilikuwa mapema tu yapata saa mbili hivi juu ya alama jioni. Katika meza moja ya zile zilizokuwa katikati kati ya meza zingine walikaa watu wawili wa jinsia mbili tofauti. Mwanaume na mwanamke wote vijana kabisa wakiendelea na mazungumzo yao yaliyoonekana kuwa na unyeti wa aina yake kutokana na namna walivyoilinda meza yao kila mtu baki alipokaribia kuvamia himaya yao. Hawakutaka kuungana na mtu mwingine hapo mezani pamoja na kwamba vilisalia viti viwili vitupu katika meza yenye viti vinne.
Watu hawa wawili pekee ndio hawakuwa wakitumia chochote si chakula wala kinywaji, hata mhudumu alipozuru meza yao hawakuonyesha nia kuhitaji huduma. Hali ikaendelea hivyo kwa muda mfupi kabla hajaongezeka mwanadada mwingine mwenye wajihi wa 'kimjini mjini' kuungana watu hawa mezani pao, ni dhahiri kwamba ndiye waliyekuwa wakimsubiri kwa muda wote huo ndio sababu hawakutaka aongezeke mtu mwingine kwenye viti viwili vilivyobaki vitupu asiye katika mpango wao. Mwanadada huyo alipofika eneo hili akatumia muda mfupi akiangaza huku na kule alipowatambua wenyeji wake akajongea katika meza yao na kuketi, yeye pia hakuagiza chochote kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake na alionekana mwenye haraka sana. Aliketi mbele ya meza akitazamana na wenyeji wake huku ameipa mgongo bendi ambayo iliendelea kutumbuiza taratibu kwa kuchanganya mahadhi.
Baada ya kutulia katika kiti chake mazungumzo yao yakashika hatamu. Kwanza alianza kuzungumza dada huyu mjanjamjanja, aliongea kwa haraka alipomaliza akaacha nafasi kwa wenyeji wake kuzungumza yao. Ni mazungumzo ambayo hakuna aliyeyasikia kutokana na pilikapilika za mahali hapa zenye kumfanya kila aliyepo kujali zaidi mambo yake, isitoshe watu hawa watatu walihakikisha hakuna mtu mwingine zaidi yao angesikia mazungumzo yao, kuna wakati iliwalazimu kuinama kidogo na kusogeleana ili kusikilizana vyema au wakati ambao mhudumu angefika jirani nao wangesitisha mazungumzo mpaka pale akishaondoka wanaendelea tena.
Mazungumzo yakaendelea katika umakini uleule na sasa yule dada alionekana kama anayepokea maelekezo fulani kutoka kwa wenyeji wake. Dakika kumi tu tangu yule mwanadada afike mahali hapo zilimtosha kufanya kilichomleta hivyo akainuka na kuondoka. Wenyeji wake walipohakikisha ameshatokomea hawakudumu kwa muda mrefu wakaondoka pia!
****
Sold by: Lackson Tungaraza
Sold by: Lackson Tungaraza
Sold by: Lackson Tungaraza