BIASHARA NA UJASIRIAMALI
Tunapozunguzia biashara na ujasiriamali kila mmoja ana mtazamo wake wengine wanaweza kuangalia katika upande wa kuwa sehemu ya kutoka kimaisha mwingine anaangalia katika upande mwingine mgumu wa kutokutoka kimaisha.Swali la kujiuliza je kila mmoja anaweza kuwa mfanyabiashara au mjasiriamali? Na wewe vipi unadhani unatakuwa kuwa mfanyabiashara na mjasiriamali? Sifa za mjasiriamali na mfanyabiashara ni zipi haswa? Maswali haya yote yatajibiwa ipasavyo katika kitabu hiki pindi unapokisoma mpaka mwisho.
Katika maisha ili uweze kusonga mbele ni lazima uamue kupiga hatua tena kwa uthubutu mkubwa haswa kama unataka kuona ndoto zako zinatimia, lakini kitu ambacho kinawakwamisha wengi ni asilimia kubwa ya Akili zao kutokuziweka katika hali ya ushindi. SOCRATES Mmoja kati ya wanafalsafa wakubwa Duniani alishawahi kusema hivi: “Siwezi kumfundisha mtu kitu chochote. Ila Ninaweza kumfundisha mtu jinsi ya kuwaza.”
Kuwa na Akili ya ushindi ni pamoja na kuwa na imani ya kufanikiwa kwa mambo yako hata kama uko katika nafasi ambayo unaona hakuna uwezekano wa kufanikiwa. Akili ya Ushindi ni pamoja na kujenga ari ya ushindi katika akili yako, kwa kurahisisha mapambano ya kifikra kwenye nyanja tofauti za maisha nikimaanisha kwenye biashara, ujasiriamali bila kusahau kusaidia wale ambao hawana kazi au wenye kazi waweze kujitambua na kubadilisha maisha yao.
Akili ya Ushindi itasaidia waajiriwa kutambua ni namna gani wanaweza kubadilisha maisha yao na kuachana na dhana potofu za kushindwa kufanikiwa katika ajira, waajiri pia kuna mambo ambayo watapata kujua kwa namna gani wanaweza kushughulika vizuri zaidi na watu ambao wamewaajiri.
Kitabu hiki cha ‘Biashara na Ujasiriamali’ kilicho ndani ya mfululizo wa vitabu vya programu ya Akili ya Ushindi kimebeba maarifa makubwa sana ambayo yatakusaidia kila unaposoma uamshe hali ya kuweza kusababisha mambo makubwa kufanyika. Kila sura ambayo utaipitia ni lazima uondoke na kitu cha tofauti katika maisha yako, na ukiweza kukitendea kazi bila shaka utakuwa mtu mwingine kabisa mwenye akili ya ushindi kwa sababu kitabu hiki kitaenda na kutengenezea fikra ambazo mbele ya kila jambo ambalo inawezekana wengine wanalichukulia kuwa gumu kwako litawezekana, hata kama ulikuwa huwezi kuona fursa yoyote ya kuifanyia kazi, kupitia kitabu hiki lazima upate fursa ya kuanza kuifanyia kazi.
Kwa malengo ambayo unayo inawezekana kwa muda mrefu uliona kuwa malengo yako hayawezi kutimilika, kwa sababu ya jinsi akili yako ulivyokuwa umeiweka kuwazia malengo yako na mwenendo wako. Akili ndiyo ambayo inafanya maamuzi kuhusu maisha yako kutokana na vitu ambavyo unaviingiza ndani yake, na ukiona mambo hayasongi jua bado nafasi kubwa katika akili yako imetawaliwa na mambo ambayo sio sahihi au umeweka mambo sahihi lakini ukakosa nguvu ya kuweza kuyafanyia kazi.
Kitabu hiki kinaenda kukufichulia siri za mambo mengi katika maisha yako, ikiwemo watu maarufu na matajiri duniani walivyoweza kufanikiwa katika biashara zao kwa kuwa na Akili ya Ushindi.Ndoto zako na maisha yako yatabadilika kwa kubadilisha akili yako na kuiweka katika mazingira ya ushindi na sio vinginevyo.