BAYO NA IMBORI : Ladha Ya Jasho Tamu
BAYO NA IMBORI : Ladha Ya Jasho Tamu. Riwaya hii inasimulia juu ya ndugu wawili, Bayo na Imbori. Mmoja akiwa mwandishi wa habari na mwingine wakili, wanaamua kutumia taaluma zao kupambana na udhalimu uliokuwa unaendelea kwenye jamii yao. Zoezi hilo kwao halikuwa sawa na la kumsukuma mlevi. Wanaonywa kuwa: pamoja na kwamba ni janga, lakini kupinga masuala ya udhalimu kulimaanisha kugusa masilahi ya watu mashughuri na wenye kufu mbalimbali katika jamii, jambo ambalo litawaghalimu maana kilichompata peku na ungo naye kitampata. Hata hivyo, Bayo na nduguye Imbori, hawakuwa tayari kusikia la muadhini wala mnadi swala. Walikuwa tayari kuilipa gharama yoyote ile ikibidi hata uhai wao, lakini si kushuhudia vitendo hivyo vikizidi kuitafuna jamii. Na hapo ndipo moto unapowawakia. Ni moto mkubwa ambao kwa kiasi kikubwa ndio nunaotengeneza matukio ya kusisimua, kusikitisha na kufurahisha; yaliyosimuliwa kwa weledi mkubwa wa kisanaa ambao unajenga picha ya matukio yake kwenye fikra za msomaji wakati asomapo.
WASIFU WANGU: Boniphace Daud Ngumije ni mzaliwa wa jijini Mwanza, aliyejikita kwenye masuala ya fasihi kwa muda wa takribani miaka kumi sasa. Amebobea katika uandishi wa vitabu vya riwaya na mashairi ambayo huyaghani kwenye majukwaa mbalimbali kila apatapo nafasi. Vitabu vyake vingine alivyoandika ni pamoja na Ombaomba Aliyeuza Wanaye pamoja na Gaidi wa Ajabu. Hufanya pia kazi ya kuwaandikia vitabu watu wasio na nafasi, au wenye kiu na haja ya kufanya hivyo, lakini hawana utaalamu. Lakini pia ni miongoni mwa waanzilishi wa kampuni ya Simulizi Kali Africa, inayojihusisha na masuala mbalimbali ya kifasihi ikiwa ni pamoja na uchapishaji wa vitabu na uuzaji.